Historia

Mfuko wa Rais wa Kujitegemea ni Taasisi ya Serikali inayotoa mafunzo ya elimu ya; fedha, ujasiriamali na kujitegemea pamoja na mikopo kwa Vijana na Wanawake ili kuwawezesha kujiajiri na kujitegemea kiuchumi.

Wazo la kuanzisha Mfuko huu lilitolewa na hayati Waziri Mkuu Mheshimiwa Edward Moringe Sokoine kwa lengo la kuwasaidia wananchi kujitegemea kupitia shughuli za uzalishaji mali hasa katika maeneo ya kilimo,uvuvi,ufugaji na viwanda vidogo vidogo.Wazo hili lilikuwa linakusudia kutekeleza sera ya “Nguvu kazi”.

Mwaka 1983 Juni, wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti Serikali ilitangaza uamuzi wa kuunda Mfuko wa Rais wa Taifa wa Dhamana wa Kujitegemea. Sambamba na tangazo, Mheshimiwa hayati Edward Sokoine, aliamua pia kuchangia nusu ya mshahara wake katika mtaji wa Mfuko.

Mwaka 1984 Mfuko wa Rais wa kujitegemea ulianzishwa chini ya “Trustees Incorporation Ordinance, chapter 375” ya sheria za Tanzania. Mfuko uliandikishwa rasmi mwaka 1988 na kupata namba ya usajili 845.

Mnamo mwaka 1988, hayati Mheshimiwa Rais Mwalimu Julius K.Nyerere aliendeleza Sera ya Kujitegemea kupitia huduma za Mfuko huu na kuhamishia usimamizi wa shughuli za Mfuko, Ofisi ya Rais Ikulu .